skip to main |
skip to sidebar
ORANJE FOOTBALL ACADEMY YATOA PONGEZI KWA RAIS MPYA WA ZFA
Kituo cha kukuza soka kwa vijana nchini Oranje Football Academy "O.F.A" kwaniaba ya viongozi wake wa ndani na nje ya nchi pamoja na wachezaji wake wote kinatoa pongezi za dhati kwa Rais mpya wa Chama cha soka cha Zanzibar Z.F.A Aman Ibrahim Makungu kwa kuchaguliwa kwake kushika nafasi hio kuwa Rais mpya wa Soka nchini.
Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kimepata Rais mpya kufuatia mgombea pekee wa nafasi hiyo Amani Ibrahim Makungu kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani.
Makungu alimudu kuzoa kura 49, sawa na asilimia 94 ya kura zilizopigwa kutokana na wajumbe 52 wa mkutano mkuu wa ZFA, ambapo ni kura tatu tu ndizo zilizomkataa.
Katika uchaguzi huo ulioendeshwa chini ya usimamizi wa kamati ya uchaguzi ya chama hicho iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Gulam Abdallah Rashid, wapiga kura walipata fursa kumuuliza mgombea huyo masuala juu ya namna atakavyoendeleza soka la Zanzibar iwapo atachaguliwa.
Akijibu masuala hayo, na baada ya kutangazwa kwa matokeo, Rais huyo mteule alisema, kimsingi ana dhamira ya dhati kuleta mabadiliko katika soka la Zanzibar kwa wilaya zote Unguja na Pemba ili kurejesha hadhi ya visiwa hivi kisoka.
Aidha alisema anakusudia kutumia kila uwezo alionao, pamoja na kubuni njia chanya za kutafuta fedha, ili ZFA iondokane na aibu ya kuwa ombaomba na hivyo kuendesha vyema shuguli zake na kuwapa matumaini Wazanzibari.
"Pamoja na nia yangu safi katika kuleta maendeleo ya soka, ieleweke kwamba hili si jambo la mtu mmoja, tutafanikiwa kwa ushirikiano wetu sote, hivyo naomba wajumbe na viongozi wenzangu, tushirikiane katika hili", alieleza Makungu.
Makungu pia, aliwashauri wajumbe hao waridhie pendekezo lake la kutaka kuajiri mtu atakayekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ufundi na Utawala, ambaye atakuwa analipwa na chama hicho, wazo ambalo wajumbe walilipokea ingawa walisema linahitaji kujadiliwa katika mkutano mkuu kabla ya kutoa baraka.
Aliyekuwa Rais wa ZFA kabla kujuzulu Ali Ferej Tamim, alikaribishwa kuzungumza baada ya uchaguzi huo, ambapo alisema anaamini mrithi wake huo ni kijana mwenye uwezo wa kuifanya vyema kazi ya kuongoza soka hapa nchini.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwa amejiuzulu, na uzee wake, yuko tayari kumsaidia Makungu na ZFA kwa jumla, kwa ushauri juu ya njia bora za kuliimarisha soka la Zanzibar.
Nafasi ya urais wa ZFA ilikuwa wazi kwa miezi mitatu kuanzia Machi 2, mwaka huu kufuatia aliyekuwa akiishikilia kwa zaidi ya miongo miwili Ali Ferej Tamim, kujiuzulu kwa sababu za kiafya na kutingwa na majukumu ya kifamilia.
Kwa niaba ya O.F.A inamtakia mafanikio na utendaji mzuri wa kazi pamoja na kuwataka wananchi wote wapenda soka nchini kutoa ushirikiano ili kuweza kuleta mabadiliko ya soka ambapo ndio dira kubwa kwa sasa kwa viongozi wakuu wa nchini.